Joy FM
Joy FM
8 May 2026, 09:07

Lishe ni mpangilio wa kula chakula chenye virutubisho vinavyohitajika mwilini kwa ajili ya afya na ukuaji bora, kwa mwanafunzi lishe bora ni jambo muhimu sana kwa sababu humsaidia kuwa na afya nzuri, uwezo mzuri wa kufikiri, na nguvu za kutekeleza shughuli zake za kila siku.
Na Mwandishi wetu
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Stephen Janks amesema suala la lishe ni la mtambuka linalohitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kuhakikisha jamii, hususani watoto wa shule, wanapata lishe bora kwa maendeleo yao.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya lishe ya Wilaya kilichojadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe ngazi ya Wilaya robo tatu kuanzia Januari hadi machi 2026 , amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan amesaini mikataba ya utendaji kazi na wakuu wa mikoa inayowataka kuhakikisha watendaji wote wanatekeleza kikamilifu masuala ya lishe katika maeneo yao.
Amesema kutokana na umuhimu huo, Halmashauri imeendelea kusisitiza shule zote kuwa na mashamba darasa yatakayosaidia kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula, mboga mboga pamoja na matunda kwa ajili ya wanafunzi.

“Tunataka kila shule iwe na shamba darasa. Kupitia mashamba hayo wanafunzi watajifunza kilimo lakini pia watapata mazao yatakayosaidia kuboresha hali ya lishe mashuleni,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa uwepo wa bustani za mboga mboga na matunda utasaidia kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubisho muhimu vinavyohitajika kwa ukuaji na afya bora ya wanafunzi.

Amewataka wakuu wote wa vitengo kushirikiana kwa ukaribu katika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi ili kuendelea kupambana na changamoto ya swala la lishe hasa mashuleni.