Joy FM
Joy FM
1 May 2026, 16:08

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoani Kigoma limeiomba Serikali kufanya marekebisho ya sheria za utumishi wa umma ili kuondoa mkanganyiko uliopo kati ya sheria hiyo na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, hususan katika suala la uwasilishwaji wa migogoro ya kikazi kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi pamoja na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Mkoa wa Kigoma, Johnson Muyombya, wakati akisoma risala katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambapo kimkoa yamefanyika katika Wilaya ya Uvinza.

Muyombya amesema kuwa uwepo wa mkanganyiko wa kisheria umekuwa ukichelewesha au kuathiri upatikanaji wa haki kwa wafanyakazi pindi wanapokumbwa na migogoro ya kikazi, na kusisitiza kuwa kufanyiwa marekebisho kwa sheria hizo kutasaidia kuongeza ufanisi, uwazi na haki mahali pa kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mheshimiwa Balozi Simon Nyakoro Sirro, amesema Serikali imepokea maombi yaliyowasilishwa katika risala hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuhakikisha haki zao zinalindwa na ustawi wao unaimarika.

Maadhimisho ya siku ya mei mosi kimkoa yamefanyika katika wilaya ya Uvinza na yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji dira ya taifa 2050