Joy FM

Waliobeba ujauzito katika umri mdogo wapewa elimu ya ukatili Kigoma

17 June 2026, 20:49

Baadhi ya watoto wa kike walipata ujauzito katika umri mdogo wakiwa kwenye picha baada ya kupatiwa elimu ya ukatili

Elimu ya ukatili imeendelea kutolewa katika makundi mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha vitendo vya ukatili vinaisha kwebye jamii ambavyo vimekuwa vikipoteza ndoto za mabinti.

Na Lucas Hoha

Baadhi ya watoto wa kike ambao wamepata changamoto ya kubeba ujauzito katika umri mdogo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wameshukuru shirika la MALKA FOUNDATION HELPER kwa kuwapa elimu ya ujasilimali na namna ya kujilinda na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Wakizungumza na Radio Joy Fm wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo yamefanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Kigoma baadhi ya watoto wa kike wamesema shirika hilo limekuwa msaada kwao kwani linawapatia mbinu za kujikwamua kiuchumi na kujilinda dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Baadhi ya viongozi wa shirika hilo wakiwa kwenye picha na mabinti waliopata mimba katika umri mdogo, Picha na Lucas Hoha

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika hilo Bi Tabu Ally Kilonge amesema kutokana na utafiti uliofanywa na shirika hilo inaonesha kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma watoto wa kike wanabeba ujauzito katika umri mdogo, ndiyo maana wakaanzisha kampeni ya kuwafanya watoto wa kike wanajitegemea kiuchumi.

Awali Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo Afisa Tawala wa Wilaya ya Kigoma Doral Buzaile pamoja na mambo mengine amelitaka shirika la MALKA kuwa wabunifu zaidi kuwa wanapotoa elimu ya ujasilimali kwa watoto pia waangalie namna ya kuwawezesha watoto kupata elimu.

Maadhimisho ya mtoto wa Afrika Mwaka huu 2026 yanaadhimishwa yakiwa na kauli mbiu isemayo Mtoto ni malezi, Msingi wa familia bora kwa Taifa imara.