Joy FM
Joy FM
9 June 2026, 11:26

UMISETA si mashindano ya michezo pekee bali ni chombo muhimu cha kukuza vipaji, nidhamu, afya, umoja na maendeleo ya wanafunzi
Na Mwandishi wetu
Kambi ya mashindano ya UMISETA Wilaya ya Uvinza imehitimishwa rasmi huku washiriki wakielekea Wilayani Kasulu kushiriki mashindano ya ngazi ya mkoa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kupata timu zitakazoiwakilisha Mkoa katika mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Mkoani Iringa.

Akizungumza wakati wa kuwaaga washiriki hao, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Ndg. Acland Kambili, amewataka kwenda kushindana kwa nidhamu, upendo na mshikamano, huku wakizingatia maadili mema na kuendelea kuitangaza vyema Wilaya ya Uvinza.
Aidha, amesema michezo ni afya na ni jukwaa muhimu la kuibua vipaji, hivyo amewahimiza washiriki kujituma kwa bidii ili kufikia malengo ya ushindi na kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kitaifa mkoani Iringa.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mwl. Julius Kakyama, amewataka washiriki kwenda kushindana kwa kujiamini na kuhakikisha wanarejea na ushindi, akibainisha kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika.
“Nataka mwende mkashindane kwa nguvu zote na kupata ushindi ili kuibua vipaji vitakavyopata nafasi ya kushiriki mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Iringa. Maandalizi yote ya msingi yamezingatiwa, hivyo mkawe mabalozi wazuri wa Uvinza,” amesema Mwl. Kakyama.
Washiriki hao wanatarajiwa kuwakilisha Wilaya ya Uvinza katika michezo mbalimbali ya UMISETA ngazi ya mkoa, wakilenga kufanya vizuri na kufuzu hatua ya kitaifa.