Joy FM
Joy FM
3 July 2026, 15:42

Amani ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote na bila amani, shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa haziwezi kufanyika kwa ufanisi
Na Hagai Ruyagila
Wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wamehimizwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na utulivu wa nchi.
Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako, alipokuwa akizungumza na wananchi katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Kasulu.
Profesa Ndalichako amesema kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kulinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Amesema amani ni tunu ya taifa inayopaswa kuthaminiwa na kulindwa na kila Mtanzania.

Aidha, amesema Tanzania imeendelea kuwa kimbilio la wananchi kutoka baadhi ya nchi jirani zinazokabiliwa na migogoro na ukosefu wa amani, hali inayoonesha umuhimu wa kuendelea kuilinda na kuiendeleza amani iliyopo nchini.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wamesema wataendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa serikali kwa kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani, ili kuhakikisha usalama na utulivu vinaendelea kudumishwa.
Wito wa viongozi pamoja na mwitikio wa wananchi unaonesha kuwa kulinda amani ni jukumu la kila mmoja. Ushirikiano kati ya wananchi, Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kudumisha utulivu, kuimarisha maendeleo na kuhakikisha ustawi wa taifa.