Joy FM

Kigoma yazindua mkakati wa usafi wa mazingira 2026/2029

18 June 2026, 19:28

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa katika uzinduzi wa mkakati wa usafi wa mazingira, Picha na Mwandishi wetu

Usafi wa mazingira ni muhimu kwa afya ya jamii kwani husaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amezindua mkakati wa Usafi wa Mazingira kwa Mkoa wa Kigoma unaolenga kuweka mwelekeo wa kudumisha  Mazingira safi na Salama pamoja na afya nora kwa wakazi mkoani huu.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa katika picha na wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma na baadhi ya viongozi, Picha na Mwandishi wetu

Mkakati huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa Juni, 2026 hadi Juni, 2029, ambapo miongoni mwa malengo yake ni kupunguza magonjwa yanayohusiana na uduni wa usafi na usalama wa maji kama vile kipindupindu, kuhara, homa ya matumbo (typhoid) na magonjwa mengine ya mlipuko.

Akizungumza wakati akizindua Mkakati huo,  Balozi Simon Sirro amesema iwapo Mkakati huo utatekelezwa kwa ufasaha, utasaidia kuwezesha wananchi kupata maji safi kwa umbali mfupi, uwepo wa vyoo bora na vya kudumu pamoja na kuhakikisha miji inakua safi wakati wote.

Nesphory Sungu Afisa Usafi na Mazingira Mkoa wa Kigoma, amesema mpaka sasa mkoa una Asilimia 65 za vyoo bora, eneo la unawaji mikono mafanikio ni asilimia 34 huku wananchi wengi wakiendelea kutumia maji yasiyo safi na Salama, hali inayosababisha kuendelea kuwepo kwa maradhi ya tumbo na yale ya mlipuko.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa na baadhi ya wadau baada ya uzinduzi wa mkakati huo, Picha na Mwandishi wetu

Mkakati wa Usafi wa Mazingira Mkoa wa Kigoma umelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za usafi wa mazingira katika kaya, taasisi za umma, shule na vituo vya afya.

Aidha malengo mengine ni kutokomeza kabisa vitendo vya kujisaidia haja kubwa ovyo, kuboresha usalama wa maji ya kunywa kupitia ulinzi wa vyanzo vya maji, usimamizi wa ubora wa maji na matumizi salama ya maji ngazi ya kaya.

Sambamba na hayo, Mkakati huo umelenga kupunguza magonjwa yanayohusiana na maji na usafi duni, kudumisha unawaji wa mikono kwa sabuni, kuimarisha usimamizi wa taka ngumu na majitaka, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi, mashirika ya kiraia na jamii katika utoaji na usimamizi wa huduma za usafi pamoja na ufuatiliaji na uwajibikaji wa wadau wote wa sekta ya usafi na maji katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri.

Mkakati huo unatekelezwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na OWM-TAMISEMI pamoja na UNICEF.