Joy FM

Mwili wa mtoto waopolewa ndani ya bwawa la Katosho

2 October 2023, 15:27

Wananchi wa mtaa wa Butunga kata ya Kibirizi manispaa ya Kigoma Ujiji wakishuhudia mwili wa mtoto ulioopolewa katika bwawa la Katosho, Picha na Hamis Ntelekwa

Wazazi na walezi mkoani Kigoma wametakiwa kuwa karibu na watoto wao ili kuhakikisha hawachezei sehemu hatarishi ikiwemo madimbwi na mabwawa.

Na Josephine Kiravu

Mwili wa mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 11 hadi 13 ambaye hajatambulika jina lake umeopolewa ukiwa unaelea ndani ya maji katika bwawa la Katosho lililopo mtaa wa Butunga kata ya Kibirizi manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mwenyekiti wa mtaa wa Butunga Hamisi Yasini amethibitisha kuopolewa kwa mwili huo ambapo inasidikika huenda marehemu akawa amezama bwawani hapo siku ya Jumamosi kwani kulikuwa na kundi kubwa la watoto waliokuwa wanaogelea na hapa anatoa neno kufuatia tukio hilo.

Sauti ya Mwenyekiti wa mtaa wa Butunga
Bwawa la Katosho ambalo ndipo mtoto mwenye miaka 11 alipozama na kufariki

Hata hivyo hadi kufikia majira ya mchana hii leo bado mwili huo ulikuwa haujatambulika na hapa Afisa Mtendaji wa kata ya Kibirizi Richard Magai anawasihi wazazi kuwa na desturi ya kuwa karibu na watoto wao ili kufahamu changamoto zao na wapi walipo.

Sauti ya mtendaji wa Kata ya Kibirizi

Nao baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mlinzi wa kitalu cha Michikichi Rajab Haruna pamoja na Ashura Hamimu wameeleza kile walichokishuhudia huku wakiwataka wazazi kuacha uzembe katika malezi ya watoto.

Sauti za mashuda

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa wa butunga hili ni tukio la pili kwa mtoto kuzama maji katika utawala ambapo amesema hali hii mara nyingi inasababishwa na wazazi kuendekeza shughuli zao na kuwaacha watoto wakiwa wanajilea wenyewe.