Joy FM

Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya Kakonko

25 January 2024, 09:15

Makamu  Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa Rehema Sombi Omary, amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, itaendeleza kazi ya kuboresha huduma za afya nchini kwa kutenga fedha na kuzishusha chini kuwafikia walengwa ambao ni wananchi.

Komredi Rehema Sombi amesema hayo mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa wodi tatu mpya katika hospitali ya wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, na kueleza kuridhishwa na namna fedha za serikali zilivyotumika vizuri.

Akitoa taarifa ya mradi kwa makamu mwenyekiti wa UVCCM Taifa Rehema Sombi, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Kakonko Dr. Frederick Mshana, amesema ujenzi wa wodi tatu mpya katika hospitali hiyo ulianza mwaka wa fedha 2022/2023 baada ya kupokea fedha Shilingi milioni 750 kutoka serikali kuu.

Baadhi ya akina mama akiwemo Salome Kitandala na Stela Francisco waliofika kupata huduma wamezungumzia hali ya huduma katika hospitali hiyo kuwa imeboreshwa.

Makamu  mwenyekiti wa UVCCM Taifa Rehema Sombi Omary, pia amekagua mradi wa ujenzi wa stendi kuu ya mabasi wiayani Kakonko ambao ulianza kujengwa tangu mwaka 2019 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 4, kisha baadaye kuhitimisha ziara yake wilayani Kakonko kwa kuzungumza na wana CCM ambapo amesifu ushirikiano baina yao na serikali.