Joy FM

Kuwashinikiza watoto wa kike kufeli bado ni tatizo Kigoma

6 March 2024, 08:44

Wazazi na walezi wa halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuacha tabia ya kuwapa maelekezo watoto wao wa kike kujifelisha katika mtihani wa taifa wa darasa la saba ili wasipate nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza.

Wito huo umetolewa na Kaimu Afisa elimu msingi Michael Mahewa wakati akizungumza na wakazi wa kata zote za halmashauri ya Mji Kasulu katika eneo la kata ya Kigondo Wilayani Kasulu Mkoani hapa.

Mahewa amesema hali hiyo haipendezi katika jamii kwani mtoto wa kike nae ni mtoto na anahaki ya kupata elimu kama ilivyo kwa mtoto wa kiume

Amesema tabia hiyo haipaswi kuendelea katika jamii kwasababu wapo viongozi wanawake ambao wamepata elimu na sasa wamekuwa chachu ya mafanikio katika ujenzi wa familia, jamii na serikali kwa ujumla.

Aidha Mahewa amesema watoto wakike wanaopewa maelekezo ya kufanya vibaya na wazazi wao wakati wakujibu mtihani wa taifa wa darasa la saba waachane na tabia hiyo ili wawe mfano wa kuigwa katika jamii inayo wazunguka

Kwa upande wao baadhi ya wazazi akiwemo Gabriel Sindagi, Uzia Gabriel na George Mamboleo kutoka halmashauri ya Mji Kasulu wamesema ni vizuri serikali ikaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuondoa upendeleo kwa mzazi kumpendelea mtoto wa kiume kwani wote ni watoto na wanahaki ya kupata elimu.