Joy FM

“mtu mwenye akili timamu hawezi kufanya ukatili”

20 March 2024, 09:13

Serikali ya Tanzani imeshauriwa kuendelea kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika jamii ili kupunguza na kutokomeza vitendo vya ukatili hali itakayosaidia kujua usawa wa mwanamke na mwanaume ndani ya jamii.

Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika Mchungaji Canon Joram Ntakije yenye makao makuu wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wakati akizungumza na redio Joy FM baada ya ibada takatifu nje ya kanisa la Kristo mfalme anglikana Murusi.

Amesema kukosekana kwa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa baadhi ya jamii imepelekea baadhi ya familia kutokuwa na uelewa kuhusu usawa wa haki ya mwanamke na mwanaume sambamba na malezi yanayotolewa katika familia zao.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kanda ya Murusi Mchungaji na Canon Laurent Magogwa  Mchungaji kiongozi wa kanisa la Kristo Mfalme Anglikana Murusi amesema jamii imekuwa ikijihusisha na masuala ya ukatili wa kijinsia kutokana na kutomjua Mungu na kutojua sheria za nchi.

Nao baadhi ya wananchi wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu pamoja na adhabu kali katika jamii ili kupinga  na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.