Joy FM

Serikali yabaini uwepo wa maabara bubu Kasulu

11 March 2024, 15:36

Wananchi wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kufuata huduma za afya katika vituo vinavyotambuliwa na serikali baada ya kubainika uwepo wa maabara Bubu ambayo imekuwa ikitoa huduma za vipimo  kinyume cha sheria.

Akiwa katika ukaguzi wa usafi wa Mazingira katika mtaa wa Luturi kata ya Mrusi Afisa mtendaji wa kata hiyo Bw.Omary sebabili akiwa ameambatana na afisa afya wa kata hiyo walibaini uwepo wa maabara Babu  ambayo mwonekano wake wa nje ukawashawishi kuingia ndani  kwa ajili ya kujiridhisha na huduma zinazotolewa.

Bw.Sebabili amesema maabara hiyo ilianza kutoa huduma mwanzoni mwa mwaka jana 2023 na ameeleza namna walivyobaini uwepo wa maabara bubu katika kata yake ambayo inatajwa kuanzishwa kwa lengo la kunufaisha duka la dawa ambalo lipojilani na maabara hiyo.

Mratibu wa huduma za maabara halmashauri ya mji Kasulu Bw.Oswadi kilula amesema katika uchunguzi ambao wameufanya kwenye maabara  hiyo wamebaini uwepo wa dawa zenye nembo ya serikali pamoja na uwepo wa majibu batili ya vipimo vinavyotolewa na mhudumu wa kwa wagonjwa wanaofika kupatiwa na matibabu.

Kwa upande wake mfamasia wa halmashauri ya mji kasulu Bw.Erick mwijage amesema wamechukua hatua ya kufunga maabara hiyo pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wa maabara hiyo ambaye pia ni mmiliki wa duka hilo la dawa 

Mmoja wa wananchi ambaye amefika kupata huduma za vipimo katika maabara hiyo ameshangazwa kuona maabara ikifungiwa kutoa huduma mbele yake wakati akiwa ameshapatiwa majibu ya ugonjwa wa mwanae.