Joy FM

Wadau wa elimu Kigoma watakiwa kusaidia kuboresha miundombinu

4 October 2023, 11:01

Mawati yaliyotolewa na Familia ya Moshi Kilima, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali imeomba wadau wa elimu kuendelea kusaidia katika kuboresha miundombinu ya elimu Mkoani Kigoma.

Na Hagai Ruyagila

Wadau wa elimu mkoani Kigoma wametakiwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu kwa kuchangia upatikanaji wa miundombinu bora kwa shule za msingi na sekondari.

Wito huo umetolewa wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madawati 40  yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3 kwa shule ya msingi Mvugwe halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kutoka kwa familia ya Moshi Kimila ambaye ni mfanyabiashara wilayani kasulu.

Akipokea madawati hayo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mvugwe Marystella Ndigeza ameishukuru familia ya Moshi Kimila kwa msaada walioutoa huku akibainisha kuwa bado wana uhitaji wa kuendelea kusaidiwa kutokana na changamoto walizonazo.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mikidadi Mbaruku licha ya kuishukuru familia ya Kimila amesema halmashauri bado ina uhaba wa madawati lakini serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wataendelea kutatua changamoto hiyo.

Shule ya msingi Mvugwe imeanzishwa mwaka 1969 ina jumla ya wanafunzi takribani 2600 na ilikuwa na upungufu wa madawati 245, na kwa msaada huo uliotolewa na familia ya Moshi Kimila umesaidia kupunguza uhaba wa madawati mpaka kufika 205.