Joy FM

Wakulima wa kahawa walia na ukosefu wa viwatilifu kakonko

18 April 2024, 14:02

Mkulima wa kahawa Wilayani Kakonko akiwa shambani anavuna kahawa, Picha na James Jovin

Licha ya elimu ya namna ya kulima kilimo chenye tija kwa wakulima walio wengi nchini lakini bado kilio cha wakulima ni kuona serikali inaboresha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Na James Jovin, Kigoma

Wakulima wa Zao la Kahawa Wilayani Kakonko Mkoa wa Kigoma wanakabiliwa na Changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na Pembejeo za Kilimo, Viwatilifu na elimu bora ya Kilimo hicho.

Baadhi ya wakulima Katika Kata ya Lugenge wilayani Kakonko wamesema kutokana na zao hilo kuwa geni kwao bado wanahitaji elimu zaidi ya kilimo hicho lakini pia  wameiomba serikali kusaidia kufikisha Pembejeo kwa wakati ili kuepuka hasara.

Sauti ya wakulima wa kahawa wilaya ya kakonko

Kwa upande wake Faustin John Afisa Kilimo Wilaya ya Kakonko amesema idara ya kilimo imejipanga kusaidia Wakulima hao hasa kuwaunganisha na Vyama  vya ushirika ili waweze kukopa Viatilifu huku Deusdedit Kilombo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Nchini amesema wamekuwa wakitoa Mbegu ambazo zinavumilia Magonjwa na kuhamasisha wadau kutoa pembejeo kwa wakati

Sauti ya afisa kilimo kakonko

Aidha mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti wa kahawa Tanzania bw. Kilombo  aliendelea kusema kuwa  Licha ya Changamoto zilizopo Taasisi yake imekuwa ikijitaidi kuzitatua na kueleza kwa sasa uzalishaji umeongezeka tofauti na miaka ya nyuma ambapo miaka miatu iliyopita walizalisha Tani 50,000 na mwaka jana 2023 walizalisha tani 80,000.

Sauti ya Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti Tanzania

Katika Wilaya ya Kakonko hadi sasa kuna wakulima wa zao la Kahawa wapatao elfu nane tu huku ikikadiliwa kuwa kufikia mwaka 2027 wakulima wa kahawa katika wilaya hiyo watakuwa zaidi ya elfu kumi na tano watakaoweza kuzalisha kahawa zaidi ya tani laki mbili kila mwaka.