Joy FM

Vibao vya anuani za makazi vyageuzwa vyuma chakavu Kigoma

14 March 2024, 10:20

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigoma Mganwa Nzota amekemea tabia za wananchi wanaoharibu miundombinu ya nguzo na vibao vya anuani ya makazi na kutumia kama vyuma chakavu.

Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi kwa maafisa watendaji wa Klkata, mitaa na wenyeviti wa mitaa katika ukumbi wa Redcross yanayotolewa na wataalam kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari.

Mh. Nzota amewataka maafisa watendaji wa kata, mitaa na wenyeviti wa serikali za mitaa kushirikiana na wananchi kuwabaini waharifu na kuwachukulia hatua katika kuharibu miundombinu ya postikodi.

Akiwasilisha mada Mtaalamu wa Mfumo wa Anuani za Makazi kutoka Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Charles Watson Gombo amesema lengo la zoezi hilo ni kusasisha taarifa na miundombinu iliyofanyika kwa kipindi kilichopita,  kuhuisha na kukusanya taarifa mpya.

Amesema mafunzo hayo yanatarajia kufanyika kwa muda wa siku mbili na zoezi la uhakiki wa taarifa ukifanyika kwa siku kumi na mbili kwa kushirikisha viongozi hao na wananchi katika mitaa sitini na nane (68) ya Manispaa Kigoma Ujiji.

Utambuzi na uwekaji wa anuani za makazi nchini ulifanyika na unafanyika kwa kutoa namba ya anuani (namba ya jengo, au kiwanja),  majina ya barabara au kitongoji na postikodi.