Joy FM

Uchumi wa wavuvi Kigoma kuchochewa na vifaa vya kisasa walivyokabidhiwa

20 November 2023, 13:55

Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akikabidhi baadhi ya vifaa vya uvuvi. Picha na Daniel Amando.

Baadhi ya wavuvi wanaofanya shughuli za uvuvi ndani ya  Ziwa Tanganyika  mkoani  Kigoma wanatarajia kujikwamua kiuchumi  baada ya serikali kuwawezesha zana za kisasa za uvuvi  ikiwemo  boti 9 na vifaa vyake zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500.

Na, Lucas Hoha

Wakizungumza  na  kituo hiki mara baada ya kupatiwa zana hizo baadhi ya wavuvi hao wamesema kupata vifaa hivyo watafanya kazi yenye tija tofauti na zamani   walipokuwa wanatumia zana zilizopitwa na wakati na kuwafanya kupata mazao madogo ya samaki

Awali akikabidhi zana hizo, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Pastory Mnyeti  amesema Serikali imejipanga kuwawezesha wananchi katika makundi tofauti  huku akitoa wito kwa Maafisa Uvuvi kuacha tabia ya kuwachonganisha wananchi na Serikali bali wajikite kutoa Elimu kuhusu Uvuvi haramu.

Kwa Upande wake,  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya mifugo na  Uvuvi, Tanzania  Agnes Meena amesema zana hizo za Uvuvi wanazitoa kwa kushirikiana na Benki ya maendeleo ya Kilimo Tanzania  na  mpaka Jumla ya boti 160 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 11.5 zitatolewa kwa awamu ya kwanza kwa wavuvi nchini.

Akizungumza  kwa  niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,  Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu katika Mkoa wa Kigoma katika sekta ya Barabara, Elimu, maji Uvuvi na kilimo na kuwa Mkoa huu utakuwa ni lango la kufanyia biashara na kukuza uchumi wa nchi za Congo na Burundi.