Joy FM

Watoto zaidi ya laki 4 kupatiwa chanjo ya surua, rubella

13 February 2024, 10:54

Zaidi ya watoto laki nne na elfu themanini na sita mia saba sabini na mbili  wenye umri wa kuanzia miezi 9-59 Mkoani Kigoma wanatarajia kupatiwa chanjo ya Surua Rubella kuanzia Feb 15-18 mwaka huu kwenye vituo vya afya na zahanati pamoja na maeneo ya mkusanyiko wa watu.

Hayo yameelezwa na mratibu wa chanjo Mkoa wa Kigoma Yohannes Mwitanyi katika kikao na kamati ya afya ya msingi mkoani hapa ambapo amesema kampeni hiyo imekuja mahususi kwa ajili ya kuongeza kinga kwa watoto dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa surua.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma Dr. Jesca Leba amewataka wazazi kutowaficha watoto wao na badala yake wajitokeze kwa wingi ili kuongeza kinga kwa watoto wao.

Mgeni rasmi katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli kwa niaba ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ameeleza umuhimu wa kampeni hiyo ya chanjo ya surua Rubella na kwamba ili kuwa na taifa imara lazima kuanza na watoto kwa kuhakikisha afya zao zinakuwa imara.

Kwa mujibu wa Mratibu wa chanjo mkoa wa Kigoma Surua Rubella ni maradhi amabyo yanaweza kukingwa kwa chanjo na magonjwa haya husababisha madhara makubwa kwa afya za watoto walio chini ya miaka mitano na hata vifo huku akieleza Pia ni lazima wagonjwa wote wenye dalili za homa na vipele ni lazima watolewe taarifa.