Joy FM

Wafanyabiashara Kigoma watakiwa kufuata kanuni na sheria za BoT

20 October 2023, 15:41

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma Filemon Makungu akitoa neno wakati wa semina kwa wafanyabiashara na viongozi wa polisi iliyoandaliwa na Benki kuu ya Tanzania BoT, Picha na Lucas Hoha

Wafanyabiashara mkoani Kigoma wametakiwa kufuata sheria za kubadilisha fedha za kigeni ili kuepuka kuingia kwenye migogoro na kuhujumu uchumi.

Na, Lucas Hoha.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma ACP Filemon Makungu amewataka wafanyabiashara wanaofanya biashara ya kubadilishana fedha za kigeni kufuata kanuni na sheria zinazotolewa na Benki kuu ya Tanzania ili kuepuka adhabu ikiwemo kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi.

Makungu ametoa wito huo wakati  Semina iliyowakutanisha baadhi ya viongozi  kutoka Benki kuu ya Tanzania, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma na wafanyabiashara iliyolenga kuwajengea uelewa juu ya kanuni mpya za biashara ya kubadilishana fedha za kigeni ya Mwaka 2023.

Naye  Afisa kutoka Benki kuu ya Tanzania kitengo cha masuala ya biashara ya kubadilishana fedha  Omary Msuya amesema baada ya kanuni hizo mpya mtu hataruhusiwa kufanya biashara ya kubadilishana fedha bila ya kusajiliwa na benki kuu, huku akiwataka wananchi kuacha kuamini biashara za kubadilishana fedha zinazofanyika kwenye mitandao ya kijamii.

Viongozi wa Polisi Kigoma wakiwa katika Picha ya Pamoja na wafanyabiashara na Viongozi wa Benki kuu ya Tanzania, Picha na Lucas Hoha

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara mkoa wa Kigoma wameomba serikali kuweka mazingira rafiki kwa wananchi juu ya namna ya kufungua maduka ya kubadilishana fedha za kigeni ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza uchumi wa mkoa wa Kigoma.