Joy FM

RUWASA yatatua kero ya maji Buhigwe

8 November 2023, 17:53

Wizara ya Maji Kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, wamefanikiwa kufikia asilimia 72.2 ya usambazaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, na kupunguza kwa kiwango kikubwa cha ukosefu wa maji wilayani humo ambapo vimebaki vijiji vitatu pekee, ambavyo havina huduma.

Na, Kadislaus Ezekiel

Akizungumza na Radio Joy kaimu Meneja Ruwasa Wilaya ya Buhigwe Frances Moreli amesema, mafanikio hayo ya kumtua mama ndoo kichwani, ni juhudi za serikali ya awamu ya sita kwa kuridhia kutoa fedha za ujenzi wa miradi katika vijiji ambavyo havikuwa na huduma ya maji, pamoja na TARURA kuhakikisha wanatekeleza miradi kwa wakati.

Kuhusu kuongeza mtandao wa maji kwa vijiji vitatu ambavyo havina huduma ya maji safi na salama, Bw. Moreli amebainisha kuwa, katika bajeti ijayo watahakikisha wanaongeza mtandao na kufanya vijiji vyote kuwa na huduma ya maji na yenye kutoshereza.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi, wamepongeza na kushukuru kusogezewa huduma ya maji, na kwamba kabla ya uwepo wa miradi ya maji, walitumia muda mwingi kufuata maji kwenye mito na visima, ambayo hata hivyo hayakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.