Joy FM

RC Kigoma apiga marufuku ramli chonganishi

18 August 2023, 10:21

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali msataafu Thobias Andengenye. Picha na KGPC

Na, Tryphone Odace

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye amewataka viongozi wa Serikali za mitaa kuchukua hatua za kisheria haraka kwa watu wanaojihusisha na upigaji wa ramli chonganishi kwani imekuwa chanzo cha kuvuruga amani na utulivu kwenye jamii.

Mh. Andengenye amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ramli chonganishi na kuwa Serikali itawafutia leseni waganga wote wa jadi ambao wamekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.

Aidha amewataka viongozi wote kusimama ipasavyo na kushirikiana ili kuhakikisha vitendo hivyo vinaisha na wananchi kuendelea kufanya shughli za maendeleo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Sheria ya tiba asili ya mwaka 2022 pia imepiga maarufuku kwa waganga wa jadi kutojihusisha na upigaji wa ramli chonganishi kwani huchochea uhasama kwa wananchi nakusababisha taharuki.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wanaomba Serikali kuchukua hatua kwani wapiga ramli wengi wamekuwa ni matapeli kwa kuwatoza faedha kwa kigezo kuwa wanakuja kuwasaidia kukabiliana na vitendo vyaushirikiana.

Matukio ya upigaji ramli chonganishi kwenye jamii yanayofanywa na kundi la watu maarufu lambalamba katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma yaliibuka hivi karibuni na kusababisha mali za watu kuharibiwa na mtu mmoja kufariki.