Joy FM

Vyama vya siasa kushirikishwa vyanzo vipya vya mapato Kasulu

28 February 2024, 08:58

Watendaji wa kata zilizopo ndani ya halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwashirikisha madiwani na viongozi wa vyama vya siasa pindi wanapoanzisha vyanzo vipya vya mapato katika kata zao.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilayani Kasulu Mberwa Chidebwe wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Mji Kasulu

Amesema mkakati walionao wa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato kwa ajili ya kuongeza mapato katika kata zao ni mzuri lakini inapendeza wakiwashirikisha madiwani, wenyekiti wa mitaa na viongozi wa chama kinachounda serikali ili kuondoa changamoto ambazo vinaweza kujitokeza kwa wananchi.

Kwa upande wao baadhi ya watendaji wa kata akiwemo Shabani Ramadhani Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwilamvya na Omary Sebabili Afisa Mtendaji wa Kata ya Murusi wamesema wamepokea maagizo hayo maana hao ni wadau muhimu ambao wanasaidia kwa kiasi kikubwa shughuli wanazozifanya ziweze kufanikiwa.