Joy FM

Kamati za maafa Kigoma, kivu na Tanganyika zakutana kuweka mikakati

22 February 2024, 09:53

Kamati za Maafa Mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa ya Kivu Kusini na Tanganyika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimekutana ili kubadilishana mbinu, kujadili na kuweka mikakati ya pamoja yenye lengo la kukabiliana na majanga katika ukanda huo. 

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye (katikati) akiwa na baadhi ya wadau kutoka mikoa jirani.

Akifungua Mkutano uliozikutanisha Kamati hizo uliofanyika mkoani humo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema athari za majanga huwa hazina mipaka ya kijiographia hivyo ni jambo jema kwa pande hizo kuweka mikakati ya pamoja ili kuepusha au kupunguza madhara kwa wakazi. 

Ameyataja majanga ambayo yamekuwa yakiendelea kuleta athari katika ukanda huo kuwa ni ukosefu wa amani,  magonjwa ya mlipuko, ongezeko la wakimbizi, uharibifu wa Mazingira, mafuriko, kuongezeka kwa kina cha Maji Ziwa Tanganyika pamoja na ajali za mara kwa mara katika ziwa hilo. 

Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la REDESO mkoa wa Kigoma Emmanuel Solomon amesema kamati zinakabiliwa na changamoto za udhaifu kwenye usimamizi wa Sheria na Miongozo inayotungwa na serikali katika nchi hizo mbili.

Akitaja mapendekezo ya pamoja ya kikao hicho, Solomon amesema Serikali za pande zote mbili zinapaswa kutilia mkazo katika kusimamia utendaji kazi wa kamati sambamba na kuziwezesha kifedha ili zimudu kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.