Joy FM

Wananchi washauriwa kuongeza kasi ya ulaji vyakula vyenye protini

16 October 2023, 17:04

Picha ya baadhi ya viongozi kutoka UN na FAO wakiwa mkoani Kigoma katika maadhimishi ya wiki ya chakula ambayo kitaifa imefanyika mkoani Kigoma/ Picha na Hamis Ntelekwa

Serikali imeendelea kusisitiza suala la ulaji wa vyakula na unywaji wa maziwa ili kufikia matarajio ya umoja wa mataifa wa ulaji wa vyakula.

Na, Josephine Kiravu

Wananchi Mkoani kigoma wametakiwa kuongeza kasi ya ulaji wm vyakula vyenye protini na unywaji wa maziwa kwani mpaka sasa kiwango cha matumizi hayo kipo chini ikilinganishwa na matarajio ya Shirika la chakula duniani.

Oktoba 16 ya kila mwaka ni siku ya chakula duniani ambapo kwa mwaka huu ni mwaka wa 43 tangu Tanzania ilipoanza kuadhimisha siku hii muhimu ya chakula duniani.

Akihutubia mamia wa wananchi waliojitokeza katika mwalo wa kibirizi kuadhimisha siku hii Mkuu wa mkoa wa kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye kwa niaba ya Waziri wa kilimo Hussein Bashe amesema siku hii ni maalum sio tu ya kukumbushana umuhimu wa chakula kwa kila mtanzania bali ni siku ya kutoa wito wa kufanikisha uhakika wa kila mtu kuwa na chakula.

Ameongeza kuwa mahitaji ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 ni Tani 16,390,404 huku Mkoa wa Kigoma ukiwa umezalisha zaidi ya tani milioni 2 kwa mwaka 2022/2023.

Kwa upande wake Prof Mohammed Sheikh ambae ni  mkurugenzi wa utafiti, mafunzo na ugani amewataka wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwa Tanganyika kuacha kutumia uvuvi haramu ili kuendelea kupata mazao ya kutosha na kusaidia jamii kupata virutubisho vya kutosha.

Siku ya chakula duniani ambayo kitaifa imefanyika Mkoani kigoma katika viwanja vya mwalo wa kibirizi na Mwanga community centre imebebwa na kauli mbiu isemayo Kila tone la maji ni muhimu, na kila sahani ya chakula ni muhimu.