Joy FM

Waziri Ndalichako agawa mitungi 400 ya gesi Kasulu

26 September 2023, 11:41

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi mtungi wa gesi kwa mama lishe. Picha na Hagai Ruyagila.

Uamzi wa serikali kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi ni miongoni mwa mikakati ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira kwa kukata kuni za kupikia.

Na, Hagai Ruyagila

Jumla ya mitungi ya gesi 400 yenye thamani ya shilingi milioni 30 imetolewa kwa wajasiriamali, shule za msingi, sekondari pamoja na baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Mji Kasulu ili kurahisha utumiaji wa nishati safi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini Prof. Joyce Ndalichako amekabidhi mitungi hiyo kwenye makundi hayo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono matumizi ya nishati safi na kuondokana na matumizi ya nishati isiyo salama ya kuni ambayo imekuwa ikisababisha madhara kwa watumiaji.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mitungi hiyo Prof. Ndalichako amesema anatamani kuona mama lishe na baba lishe wakiinuka kiuchumi na kupitia nishati hiyo itarahisisha kazi ya upikaji chakula kwa taasisi, nyumbani na mama lishe na hivyo kuongeza kipato chao.

Nao baadhi ya wajasiriamali, wakuu wa shule za msingi na sekondari pamoja na baadhi ya watumishi kutoka halmashauri hiyo wakizungumza na radio Joy Fm mara baada ya kukabidhiwa mitungi hiyo wamemshukuru mbunge wao kwa jitihada zake ambazo zimegusa sekta zote ambapo kupitia mitungi hiyo watafanya kazi za kuuza chakula kwa ufanisi mzuri zaidi.

Meneja wa masoko Oryx ges Kanda ya Ziwa Isaac Leon amesema mtungi huo wa gesi utawasaidia kupunguza gharama za matumizi sanjari na kuwasihi baada ya matumizi kuuhifadhi eneo salama.

Waziri Ndalichako amesema kila mbunge alipewa mitungi 100 kwa ajili ya kugawia wananchi katika jimbo lake ambapo yeye alimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongezewa zaidi na kufanikiwa kupewa mitungi 400 ambayo ameikabidhi kwa wananchi wake Septemba 25, 2023.