Joy FM

Madaktari 24 kuweka kambi mkoani Kigoma

29 September 2023, 14:17

Mganga Mfawidhi Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Picha na Josephine Kiravu

Wananchi zaidi ya 3000 mkoani Kigoma wanatarajiwa kupatiwa matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wanaotarajia kuweka kambi hospitalini hapo.

Na Josephine Kiravu

Zaidi ya Madaktari bingwa 12 wanatarajia kuweka kambi Mkoani kigoma kwa muda wa siku tano kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi na kupunguza adha ya kusafiri kufuata huduma za kibingwa kwenye Mikoa ya Mwanza, Dodoma na Dar es salaam.

Akizungumzia ujio wa madaktari hao, Mganga mfawidhi hospitali ya rufaa Mkoa wa Kigoma Dr Stanley Binagi amesema kutakuwa na vipimo mbalimbali ikiwemo mionzi yaani x-ray, Utrasound na CT Scan.

Amesema lengo la kambi hiyo ni kuwafikia zaidi ya wananchi 3000 na anaamini kila mwananchi atakayefika hospitalin kwa lengo la kupata huduma atahudumiwa.

Nao baadhi ya wananchi Mkoani Kigoma akiwemo Shekhe Riziki Khamisi na Shida Bakari wamefurahia ujio wa Madaktari hao huku wakiomba kuboreshwa kwa huduma za kibingwa hospitalini hapo.

Hospitali ya rufaa ya mkoa Maweni ilianzishwa mnamo Oktoba 1972 lakini mpaka sasa kuna upungufu wa huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo na kusababisha zaidi ya shilingi Milioni 40 kutumika kila  mwezi kwa ajili ya kufanya rufaa.