Joy FM

Vijana Kigoma watakiwa kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya

18 August 2023, 10:00

Afisa Program kutoka Shirika la Maendeleo ya Vijana KIVIDEA, Picha na Tryphone Odace.

Na, Tryphone Odace

Shirika la Maendeleo ya Vijana Mkoani Kigoma,  KIVIDEA limewataka vijana kujiepusha na makundi yanayoweza kusababisha kutofikia ndoto zao kwani makundi hayo yanaweza kusababisha kutumbukia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

Hayo yameelezwa na Afisa Program wa KIVIDEA, Jackline Kitema  wakati wa maadhimisho ya siku ya vijana, ambapo amesema vijana wanaathirika na dawa za kulevya kutokana na makundi yanayowazunguka.

Amesema ili kuwanusuru na janga hilo jamii haina budi kuungana na kuwasaidia vijana kwa kuwapa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya kama ambavyo shirika hilo limekuwa likifanya kwa kuwaweka karibu na kuwapatia elimu ya kujitambua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo akizungumza katika hafla hiyo amesema, vijana wengi wamekuwa wakipoteza mwelekea na kutoaminika kwenye jamii kutokana na matumizi ya dawa za kulevya huku akiwashauri kujikita zaidi  katika kufanya kazi  ili wajiingizie kipato.

Mwakilishi wa Afisa vijana Manispaa ya Kigoma ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa wa Majengo.

Baadhi ya vijana wanaopatiwa elimu ya kujitambua katika shirika hilo wamesema, serikali na taasisi binafsi kama ilivyo KIVIDEA hawana budi kuendelea kutoa elimu ya ujuzi kwa vijana ili waweze kujipatia  kipato kupitia shughuli za uzalishaji mali.

Baadhi ya vijana wanaopata elimu ya kujitambua katika Shirika la Kividea,Picha na Tryphone Odace

Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa vijana yana madhara makubwa kiafya, ki maisha na kijaamii kwa ujumla hivyo Serikali na taasisi za dini zinapaswa kusimama kidete kulinda na kuwasaidia vijana ili wasitumbukie kwenye wimbi la matumizi ya dawa hizo.