Joy FM

DC Kigoma awataka wananchi kufanya mazoezi kujikinga na maradhi

23 October 2023, 11:30

Watumishi wa Manispaa ya Kigoma, Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Wananchi wakifanya mazoezi, Picha na Lucas Hoha

Mazoezi yanatajwa kusaidia kujenga afya na kukinga miili dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwenye jamii.

Na, Lucas Hoha.

Mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amewaasa wananchi wa wilaya ya Kigoma kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya kukimbia ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo shinikizo la damu na kisukari.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo wakati wa  bonanza la kufanya mazoezi ya kukimbia ambalo limewahusisha watumishi wa serikali wa manispaa ya Kigoma, watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma na wananchi ambalo limeandaliwa na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kigoma.

Mh. Kalli amesema mtu anapofanya mazoezi ya kukimbia, kula chakula cha kutosha na kunywa maji safi na salama  inamsaidia kufanya kazi kwa bidii na kujikinga na magonjwa na kuwa amefanya hivyo kuunga mkono viongozi wa Wizara ya Afya ambao wamekuwa wakihamasisha kufanya mazoezi.

Kwa upande wao baadhi ya  maafisa michezo walioshiriki kwenye Bonanza hilo akiwemo Afisa Michezo na Utamaduni katika Manispaa ya Kigoma Ujiji  Abdul Utimbe  amesema kutokana na umhimu wa mazoezi ya kukimbia amewaomba walimu wakuu wa shule za msingi kurudisha utamaduni wa wanafunzi kukimbia kabla ya kuingia darasani kwani inasadia mwanafunzi kuelewa masomo.

Nao baadhi ya wananchi walioshiriki kwenye Bonanza hilo wamepongeza hatua hiyo ya mkuu wa Wilaya kuanzisha mbio hizo kwani zinasaidia kuimarisha umoja miongoni mwao.