Joy FM
Joy FM
19 July 2026, 16:02

Utunzaji wa mazingira ni msingi wa maendeleo endelevu, kwani unalinda afya, uchumi na ustawi wa jamii huku ukihakikisha rasilimali za asili zinadumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo
Na Emmanuel Kamangu
Mradi wa Green Alert unaofadhiliwa na CAF America unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi unatarajia kuwafikia wakazi elfu 30 wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na kugharimu shilingi million 127 wakati wa utekelezaji wake ili kuhakikisha jamii inatambua umhimu wa kutunza mazingra.
Mwakilishi wa katibu tawala Wilaya ya Kasulu Bw. Hasan Lucas amesema hayo wakati akifungua kikao cha utambulisho wa Mradi huo wa Green Alert unaotekelezwa na Taasisi ya Tanzania Wote Equality Alliance (TAWEA) kwa ufadhili wa CAF America ambapo amewahimiza watendaji wa kata na wataalmau wa mazingira kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia taarifa za TMA katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa yao wenyewe.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo kutoka TAWEA Bw. Festo Mrina, amesema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili katika kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na unatarajiwa kuwafikia zaidi ya wananchi elfu 30 kwa kutumia jumbe fupi za simu, redio pamoja na mitandao ya kijamii.

Aidha Meneja wa Hali ya Hewa Mkoa wa Kigoma, Mugisha Kyaruzi, amesema ushiriki wa TMA katika mradi huo utasaidia kuifikishia jamii taarifa sahihi za hali ya hewa na kupunguza utegemezi wa taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
Mradi wa Green Alert ulianza Aprili 2026 na unatarajiwa kukamilika Machi 2028 ambapo utatekelezwa katika kata za Nyamidaho, Kurugongo, Makere, Kitagata na Kabulanzwili