Joy FM

Wananchi watakiwa kujianda na kilimo Kasulu

21 September 2026, 16:44

Wakulima wakiwa mafunzo, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali na wadau mbalimbali wa kilimo wamewataka wakulima kuanza kujianda na msimu wa kilimo

Na Hagai Ruyagila

Wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, wameshauriwa kujiandaa mapema kwa msimu wa kilimo kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu, pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni

Wito huo umetolewa na Afisa Kilimo kutoka Kata ya Nyasha, Maria Mwagama, wakati akizungumza baada ya semina iliyofanyika katika Chuo cha Mubondo, kilichopo Kata ya Ruhita halmashauri ya Mji Kasulu.

Mwagama amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wananchi kujenga uwezo wa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, sambamba na kuwapatia elimu kuhusu matumizi ya mbinu bora za kilimo zinazoweza kuongeza uzalishaji wa mazao.

Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Uwezo wa Wakulima katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Kupunguza Maafa na Majanga Wilaya ya Kasulu, Mohamed Karata, amesema mradi huo unalenga kuwajengea wakulima uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame.

Aidha, amesema kupitia mradi huo, wakulima wanapatiwa elimu kuhusu mbinu bora za kilim, pamoja na matumizi sahihi ya mbegu bora, hatua inayolenga kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo.

Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wamesema mafunzo hayo yamewapatia elimu muhimu itakayowasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua za El Niño, huku wakiahidi kutumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha shughuli zao za kilimo.

Mradi huo umefikia kata 10 za Halmashauri ya Mji Kasulu na unaratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake, UN Women, kwa lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo kilimo, sambamba na kuchangia juhudi za kupunguza ukatili wa kijinsia.