Joy FM

Rais wa AMECEA azindua kliniki ya macho Kasulu

9 October 2026, 14:25

Askofu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Gervais Nyaisonga, Picha na Hagai Ruyagila

Uzinduzi wa kliniki hiyo umetajwa na wananchi wa Wilaya Kasulu na maeneo jirani kama huduma muhimu kwao kwani walitembelea umbali mrefu kufuata huduma hizo

Na Hagai Ruyagila

Rais wa Mabaraza ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (AMECEA) na Askofu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Gervais Nyaisonga amezindua huduma za kibingwa za Kliniki ya macho pamoja na jengo jipya la kutolea huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Kabanga, iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu, Mkoani Kigoma.

Akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Askofu Mkuu Nyaisonga amesisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wenye changamoto za magonjwa ya macho.

Muonekano wa jengo lililozinduliwa, Picha na Hagai Ruyagila

Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Kigoma, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, amesema uwepo wa huduma hizo utakuwa chachu na manufaa kwa Wananchi kupata huduma karibu na kupunguza kutembea umbali mrefu hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wa Kigoma na maeneo mengine.

Mkuu wa Wilaya Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola, ameahidi utunzwaji wa mradi huo pamoja na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ubora unaostahili.

Meneja Mkazi wa Programu wa Shirika la Tanzaneye, Ryner Linuma, amesema ujenzi wa jengo hilo pamoja na vifaa vya kutolea huduma umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni Moja.

Amesema shirika hilo linaendelea kujikita katika kuongeza idadi ya wataalamu wa afya ya macho pamoja na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma hizo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya macho kwa wananchi.

Meneja mkazi, Picha na Hagai Ruyagila

Uzinduzi wa jengo hilo na huduma za kibingwa za magonjwa ya macho unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya macho ukisaidia kupunguza gharama na muda ambao wananchi wamekuwa wakitumia kusafiri kutafuta matibabu hayo.

Muonekano wa jengo lililozinduliwa, Picha na Hagai Ruyagila