Joy FM
Joy FM
10 November 2026, 15:33

Upatikanaji wa chakula shuleni ni muhimu kwa wanafunzi kwani inasaidia kuongeza hali ya wanafunzi kupunza utoro shuleni
Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, CPA Fred Milanzi, ametoa wito wa kuongezwa kwa elimu na hamasa kwa jamii juu ya umuhimu wa upatikanaji wa chakula shuleni kwa wanafunzi, ili kuinua kiwango cha ufaulu.
CPA Milanzi ametoa rai hiyo wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa Mwanamke na Mtoto (MTAKUWWA), kilichofanyika leo Novemba 10, 2026, katika ukumbi wa Halmashauri ya Uvinza, wakati wa uwasilishaji wa utekelezaji wa mpango huo katika robo ya kwanza ya mwaka.

Amesema utoaji wa elimu kwa jamii ni muhimu ili jamii itambue wajibu wake wa kuwapatia watoto chakula wawapo shuleni, ili kutimiza lengo la Serikali la kuhakikisha kila shule inatoa chakula kwa wanafunzi.
Aidha, amesisitiza kuwa yeyote anayeshindwa kutimiza wajibu wa kumpatia mtoto chakula lazima awajibishwe kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa mpango huo Wilaya ya Uvinza, Bi. Elly Kitta, ameeleza kuwa elimu juu ya ukatili dhidi ya mwanamke na mtoto imekuwa ikitolewa mara kwa mara katika ngazi zote, kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya madhara ya kuwaajiri watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

Amesisitiza pia watumishi kuwa mfano wa kuigwa kwa kutowaajiri watoto wenye umri wa kuwa shule na waliochini ya miaka 18.
Katika kikao hicho, wajumbe wameweka maazimio ya kuwataka wasimamizi wa mpango huo kuwa na taarifa zinazoshabiana kutoka ngazi ya chini hadi ngazi ya juu.Lengo ni kuwa na kanzidata yenye kuonesha takwimu sahihi za namna ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango huo unavyofanyika, ili iwe rahisi kubaini kasoro zinazojitokeza wakati wa utekelezaji na kuzipatia ufumbuzi.