Joy FM

RC Kigoma ataka viongozi kuwajibika

29 October 2026, 15:46

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, Picha na Hagai Ruyagila

Viongozi Mkoani Kigoma wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua

Na Hagai Ruyagila

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka viongozi wa Serikali, taasisi binafsi pamoja na watendaji wa kata, mitaa na vijiji kuwajibika ipasavyo na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino.

Balozi Sirro ametoa wito huo wakati akizungumza katika kikao cha maandalizi na utayari wa kukabiliana na athari za mvua hizo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, mkoani Kigoma.

Baadhi ya viongozi wa Serikali kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Kigoma wakiwa katika kikao hicho, Picha na Hagai Ruyagila

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wadau mbalimbali katika kuhakikisha hatua za kinga na tahadhari zinachukuliwa kwa wakati, ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi, kusafisha mifereji na mitaro pamoja na kutekeleza maazimio ya kikao hicho ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa ndani ya wilaya hiyo kujiandaa kukabiliana na athari zitokanazo na Mvua hizo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa, huku zoezi la kusafisha mitaro likiendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, Picha na Hagai Ruyagila

Awali, akisoma taarifa ya Kamati ya Maafa, Mratibu wa Maafa wa Mkoa wa Kigoma, Justin Njuu, amesema mkoa umejipanga kukabiliana na athari za mvua za El Niño, ikiwemo kuboresha miundombinu ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.

Mratibu wa Maafa wa Mkoa wa Kigoma, Justin Njuu, Picha na Hagai Ruyaila

Katika kikao hicho, viongozi wa Serikali kutoka wilaya zote za Mkoa wa Kigoma waliwasilisha taarifa mbele ya Mkuu wa Mkoa, zikieleza mipango na mikakati iliyowekwa katika maeneo yao ili kuimarisha utayari wa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

Hatua hizo zinalenga kuongeza uelewa wa wananchi, kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha hatua za kinga zinachukuliwa mapema ili kulinda maisha ya watu na mali zao dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.