Joy FM

Enable, FDC watoa madawati kwa uongozi wa Kasulu

10 November 2026, 15:17

Picha na Hagai Ruyagila

Wadau wa maendeleo wametakiwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia

Na Hagai Ruyagila

Shirika la Enabel kwa kushirikiana na chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu FDC kupitia mradi wa wezesha binti  wamekabidhi msaada wa madawati 87 kwa ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri Mji Kasulu mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya madawati hayo, mwakilishi wa Shirika la Enabel wilayani Kasulu Abel Mbilinyi amesema msaada huo umetolewa kwa lengo la kusaidia kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu na kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati katika halmashauri hiyo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Sara Mfilinge, amelishukuru Shirika la Enabel na Chuo Cha Kasulu FDC kwa msaada huo na kueleza kuwa utasaidia kuboresha mazingira ya wanafunzi katika kupata mafunzo yao.

Naye Mkuu wa chuo Cha Kasulu FDC Fridegarda Kokutungunika Mukyanuzi amelishukuru Shirika la Enabel kwa kukiamini chuo hicho na kukipatia fursa pamoja na vifaa vilivyowezesha utengenezaji wa madawati hayo.

Amesema ushirikiano huo umewezesha chuo kutumia ujuzi na rasilimali zilizopo kuzalisha bidhaa zenye manufaa kwa jamii, huku akisisitiza kuwa chuo kitaendelea kutumia ujuzi unaopatikana chuoni hapo katika kuchangia utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii.