Joy FM
Joy FM
1 July 2026, 12:13

Vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kuongeza kipato na kuimarisha maendeleo ya jamii ili vyama hivi viweze kufikia malengo yake, ni muhimu viendeshwe kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali.
Na Hagai Ruyagila
Viongozi wa vyama vya ushirika Mkoani Kigoma wametakiwa kushirikiana kwa karibu na wakaguzi wa hesabu za serikali ili kuhakikisha kunakuwepo na uwazi, uwajibikaji na usimamizi mzuri wa rasilimali za vyama hivyo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Nyakoro Sirro aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, wakati akifunga Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Kigoma iliyofanyika kwa siku mbili mjini Kasulu.

Akizungumza katika hafla hiyo, amesema ni muhimu kwa viongozi wa vyama vya ushirika kuhakikisha wanashirikiana kikamilifu na wakaguzi wa hesabu za Serikali ili kuimarisha utendaji wa vyama hivyo na kujenga imani kwa wanachama pamoja na wadau wengine.
Katibu Tawala msaidizi uchumi uzalishaji mkoa wa Kigoma, James Peter amesema Serikali inaendelea kuviunga mkono vyama vya ushirika kutokana na mchango wake mkubwa katika kuinua uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Katibu wa Basanza AMCOS, Bi. Neema Conrad, amesema vyama vya ushirika vimeendelea kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima kwa kuwatafutia masoko ya uhakika ya mazao yao, jambo ambalo limechangia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya wananchi.
