Joy FM
Joy FM
19 June 2026, 20:44

Uzinduzi wa mahakama hizo kunatajwa kusogeza huduma karibu na wananchi ambao walitumia muda mwingi kufuata huduma za mahakama mbali na maeneo yao
Na Timotheo Leonard
Mahakama za Mwanzo za Bangwe, Herujuu na Manyovu zimezinduliwa rasmi leo Juni 19, 2026 mkoani Kigoma, hatua inayolenga kusogeza huduma za sheria na haki karibu zaidi na wananchi wa maeneo hayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mgeni rasmi ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Augustine Karichuba Rwizile, amesema uwepo wa mahakama hizo unapaswa kuwa chachu kwa watendaji wa mahakama kuendelea kutenda haki kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji ili kulinda heshima ya mhimili wa mahakama.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simoni Sirro, amesema mahakama hizo zitasaidia kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za mahakama, huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na mhimili huo katika kuboresha utoaji wa haki.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Yusuph Kasuka, amesema miradi ya ujenzi wa mahakama hizo tatu umegharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha miundombinu ya utoaji haki nchini.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameipongeza serikali kwa kukamilisha miradi hiyo, wakisema itasaidia kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi na kupunguza mlundikano wa kesi katika maeneo yao.