Joy FM
Joy FM
17 July 2026, 11:35

Usajili na urasimishaji wa biashara za famasi na maduka ya dawa muhimu ni jambo la msingi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma salama na bora za afya kwa wananchi.
Na Emmanuel Kamangu
Wamiliki wa famasi na maduka ya dawa muhimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wamehimizwa kusajili na kurasimisha biashara zao kwa mujibu wa sheria ikiwa ni kuboresha huduma za afya na kuhakikisha usalama wa wananchi unazingatiwa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, wakati akifungua mafunzo endelevu ya utoaji wa huduma za famasi na maduka ya dawa muhimu ambapo amesema zaidi ya maduka ya dawa 300 hayajasajiliwa na ambayo yamesajiliwa na kurasimishwa yakiwa maduka ya dawa 33 pekee.

CPA Kafuku ameongeza kuwa kutokusajiliwa kwa maduka mengi ya dawa ni kutarisha afya za wananchi wa halmashauri ya wilaya hiyo ikiwemo kudororsha ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya wananchi.
Aidha Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Mageni Pondamali, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wamiliki wa famasi na maduka ya dawa muhimu pamoja na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao kisheria kwa kuzingatia kanuni za kiafya ili kutoa huduma kwa ufansi.

Kwa upande wake Mfamasia wa Wilaya hiyo Bw. Faustin Kasalya, amewataka wamiliki wa maduka ya dawa muhimu kuhakikisha wanauza dawa zilizoidhinishwa kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuhakiksha watumishi wanaowaajiri wanakidhi sifa na vigezo vinavyotakiwa .
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo mmoja wao akiwa Bw, Kawambwa Kawambwa ameishauri Halmashauri ya wilaya ya kasulu kuimarisha usimamizi wa ufunguaji wa maduka ya dawa ili kuepuka kendesha maduka yao katika mazingira yasiyo kidhi sifa kwa usalama wa afya za wanchi.