Joy FM
Joy FM
20 July 2026, 11:46

Licha ya ushindani uliopo katika ukanda wa Afrika Mashariki, kipaumbele cha TPA ni kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na mizigo kwa haraka na kwa ufanisi ili kuendelea kuvutia wateja
Na Mwandisshi wetu
Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea na mpango wa kupanua gati na kuboresha miundombinu ya bandari nchini ili kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo inayoongezeka na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika sekta ya usafirishaji wa baharini.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema mpango huo unajumuisha kuongeza zaidi ya gati 10 katika Bandari ya Dar es Salaam, kuanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na kujenga gati tatu mpya katika Bandari ya Tanga.
Mbossa amesema pia kuna mipango ya kujenga gati mpya katika bandari nyingine nchini ili kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo kwa ufanisi zaidi.
Amebainisha kuwa kwa sasa Bandari za Tanzania zinahudumia mizigo inayozidi uwezo wa miundombinu iliyopo, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya wafanyabiashara kutumia bandari za nchini.
Mbossa amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa gati mpya, upanuzi wa maeneo ya kuhifadhi mizigo, uwekaji wa mitambo ya kisasa na uboreshaji wa barabara zinazohudumia bandari ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.