Joy FM
Joy FM
24 August 2026, 08:42

Ziara ya Waziri Nyansaho Mkoani Kigoma inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye umuhimu wa kimkakati, huku ikisisitiza umuhimu wa usalama, miundombinu na ustawi wa wananchi
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Rhimo Nyansaho amesema ujenzi wa kituo cha pamoja cha Forodha kilichopo Manyovu wilayani Buhigwe Mkoani hapa, kitaimarisha upatikanaji wa mapato sambamba na kudumisha usalama.
Akizungumza akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya Maendeleo ya kimkakati mkoani Kigoma Waziri Dkt. Rhimo amesema kituo hicho kitarahisisha pia utoaji wa huduma za Forodha huku akitoa wito kwa wakazi kutunza miundombinu ya kituo hicho mara kitakapoanza kutumika.

Pia amewataka wakazi wilayani humo kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa dhidi ya matukio yanayoweza kuhatarisha usalama kutokana na Wilaya hiyo kuwa eneo la mpakani.
Katika ziara hiyo, Waziri wa Ulinzi amekagua pia mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu Lot 1 (Kasulu-Manyovu yenye kilometa 58.7), ambapo ujenzi wake umekamilika kwa Asilimia mia Moja huku ikiwa kwenye kipindi cha matazamio.
