Joy FM
Joy FM
7 May 2026, 10:53

Serikali Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma kupitia Wizara ya elimu imepongezwa kwa kukamilisha ujenzi wa shule mpya ya kisasa wilayani mbayo itasaidia wanafunzi kusoma kwa bidii
Na Mwandishi wetu
Baraza la Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Mkoani Kigoma, limetoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia jitihada zake za kuimarisha sekta ya elimu kupitia ujenzi wa shule mpya ya kisasa ya Msingi Nyabwai.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mh. Alex Sylvester Baragomwa alieleza kuwa ujenzi wa shule hiyo ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi katika wilaya ya Kibondo.

Alisema kuwa shule ya Nyabwai itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa, kuongeza ari ya wanafunzi kuhudhuria masomo pamoja na kuboresha matokeo ya kitaaluma kwa ujumla.
“Tunatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Rais wetu pamoja na Mbunge wetu wa Jimbo la Muhambwe katika kuimarisha miundombinu ya elimu. Ujenzi wa shule hii ya kisasa ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha kila mtoto anapata elimu katika mazingira rafiki,” alisema.
Aidha, Mh Mwenyekiti amesema ataendelea kushirikiana na mamlaka za elimu wilayani hapo kuhakikisha shule hiyo inatumika ipasavyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Ujenzi wa shule ya kisasa ya Msingi Nyabwai umegharimu kiasi cha shilingi milioni 347 na ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kuongeza ubora wa miundombinu na upatikanaji wa huduma za elimu kwa wote.