Joy FM
Joy FM
10 June 2026, 14:36

Katibu tawala wa Wilaya ya Kasulu Mkoani kigoma amesema vijana hawana budi kutumia mikopo inayotolewa na serikali iweze kuwasaidia kujiingizia kipato kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali
Na Hagai Ruyagila
Vijana wa Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na serikali kupitia Halmashauri mbalimbali nchini ili kusaidia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Wito huo umetolewa na Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtewele, ambaye amesema mwitikio wa vijana kuomba mikopo hiyo bado ni mdogo, hali inayochangia baadhi yao kuendelea kuwa tegemezi katika jamii badala ya kujitegemea kiuchumi.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Kasulu, Rebecca Mpango, ameeleza sheria, taratibu na vigezo vinavyotakiwa kufuatwa na vikundi vya vijana, vinavyoomba mikopo hiyo.
Akibainisha kuwa lengo la serikali ni kuwezesha wananchi kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo na kuongeza kipato.
Baadhi ya Vijana wa wilaya ya Kasulu wamekiri kuwa mwitikio wa kuomba mikopo hiyo bado ni mdogo kutokana na kushindwa kukidhi baadhi ya vigezo vilivyowekwa na serikali, huku wakiiomba mamlaka husika kuendelea kutoa elimu ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kunufaika na fursa hiyo.
Hata hivyo serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kujiunga katika vikundi vinavyotambulika kisheria na kuzingatia masharti yote yaliyowekwa ili waweze kupata mikopo hiyo na kuitumia kama nyenzo ya kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wao.