Joy FM

NGOs zatakiwa kubuni vyanzo vya mapato Kigoma

30 June 2026, 11:39

Baadhi ya wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wakiwa katika kiako cha mashirika, Picha na Filbert Gabriel

Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yana mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na Serikali kutoa huduma mbalimbali kama elimu, afya, mazingira, haki za binadamu na ustawi wa jamii.

Na Filbert Gabriel

Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini yameshauriwa kuwa na ubunifu wa kuanzisha vyanzo vya mapato vya ndani ili yaweze kujiendesha kwa ufanisi na kuendelea kutoa huduma kwa jamii.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wakurugenzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Kigoma, Mwenyekiti wa NaCoNGO Taifa, Gaspar Makala, amesema kwa sasa upatikanaji wa fedha kutoka kwa wafadhili wa nje umepungua, hivyo ni muhimu kwa mashirika hayo kubuni njia mbadala za kujitegemea huku yakiendelea kutekeleza majukumu yake ya kijamii.

Makala amesema bado zipo taasisi mbalimbali za kifedha zinazotoa fursa za ufadhili kwa mashirika yanayotekeleza miradi yenye tija kwa jamii, hivyo viongozi wa mashirika wanapaswa kuzitumia fursa hizo ipasavyo.

Baadhi ya viongozi wakiwa wakiwa katika mkutano wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, Picha na Filbert Gabriel

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NaCoNGO Mkoa wa Kigoma, Alex Luoga, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali ni wadau muhimu wa maendeleo na yana jukumu kubwa la kuisaidia Serikali kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi, ikiwemo kudumisha amani na maendeleo ya kijamii.

Luoga ameongeza kuwa kupungua kwa fedha kutoka kwa wafadhili kunapaswa kupokelewa kama changamoto inayohitaji ubunifu na mikakati mipya ya kujiendesha, bila kuathiri utulivu wa Taifa na mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya wananchi.