Joy FM
Joy FM
26 May 2026, 14:01

Maendeleo ya jamii yoyote hutegemea uwepo wa miradi mbalimbali kama vile barabara, shule, hospitali, miradi ya maji na umeme na miradi hii huhitaji usimamizi mzuri ili iweze kutekelezwa kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Na Mwandishi wetu
Wajumbe wa kamati ya Usalama Mkoa wakiambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma wamefanya ziara ya Kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani Kakonko.
Ziara hiyo imefanyika Jumatatu 25 Mei, 2026 katika maeneo mbalimbali ikiwemo hospitali ya Wilaya, Ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji, Ujenzi wa vibanda vya kisasa awamu ya pili soko kuu la Kakonko, barabara ya lami stendi kuu ya mabasi, shule ya msingi Kihogazi, nyumba za Wakuu wa Idara, na ukarabati wa maabara katika shule ya sekondari Buyungu iliyopo kata ya Kiziguzigu.

Akihitimisha ziara hiyo mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Uhamiaji wa Mkoa, Dismas Mlula, kwa niaba ya kamati alipongeza hatua iliyofikiwa kwenye miradi hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia maelekezo na maoni yaliyotolewa katika ukamilishaji wa miradi na kudumisha ushirikiano wa pamoja kwa wadau wote wanaohusika katika utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo.

Kwa upande wake Michael Faraay, Kaimu Mkurugenzi mtendaji amewashukuru wajumbe wa kamati ya usalama ya mkoa kwa ujio wao na kueleza kuwa wamepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na kuahidi kufanyia kazi kwa vitendo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kunufaika na miradi hiyo.
