Joy FM
Joy FM
23 April 2026, 14:47

Choo katika zahanati kina umuhimu mkubwa sana, si suala la ziada bali ni hitaji la msingi kwa huduma bora za afya kwani bila choo, mazingira yanakuwa machafu na yanaweza kusababisha kuenea kwa magonjwa ya mlipuko kama kuhara, kipindupindu na maambukizi mengine.
Na Hagai Ruyagila
Diwani wa Kata ya Kurugongo, Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, Mh. Edson Hanyuma, ameiomba serikali kuongeza juhudi katika kukamilisha ujenzi wa choo katika Zahanati ya Migunga, ili kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Mhe, Hanyuma ametoa ombi hilo wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kata yake, katika mkutano wa Baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Kasulu katika kikao cha robo ya tatu cha mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema kukamilika kwa miundombinu hiyo, hususan choo, kutachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wanapohitaji huduma.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Mh. Charles Benjamini, ambaye pia aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, amesema serikali inatabua umuhimu wa kuboresha miundombinu ya sekta ya afya na imejipanga kuhakikisha ujenzi wa choo hicho unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma bora.
