Joy FM
Joy FM
22 July 2026, 17:22

Uchangiaji wa damu salama ni moja ya matendo muhimu ya kibinadamu yanayochangia kuokoa maisha ya watu wengi na damu ni rasilimali muhimu ambayo haiwezi kutengenezwa viwandani, hivyo hupatikana kupitia watu wanaojitolea kuchangia
Na Emmanuel Kamangu
Kikundi cha Kiislamu cha JAI wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, kimezindua zoezi la uchangiaji wa damu salama katika Hospitali ya Mji wa Kasulu Mlimani, likiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa damu na kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji.
JAI ni jumuiya inayojihusisha na huduma za kibinadamu, ikiwemo kuwahudumia wagonjwa, yatima na wajane. Kupitia zoezi hilo, wanachama wa jumuiya hiyo wameendelea kuonesha moyo wa kujitolea kwa kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa mbalimbali, wakiwemo wajawazito wanaohitaji huduma za dharura.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Dkt. Nangi William, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliihamasisha jamii kujitokeza kwa wingi kuchangia damu salama. Aidha, aliipongeza JAI kwa kuendelea kuonesha moyo wa kujitolea na kushiriki katika shughuli zinazogusa maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JAI wilayani Kasulu, Sheikh Abdulrahman Nyamugenda, alisema kuwa miongoni mwa shughuli kuu zinazotekelezwa na jumuiya hiyo ni utoaji wa misaada mbalimbali, ikiwemo huduma za damu, matibabu kwa watu wasiojiweza, pamoja na kuwasaidia wahitaji bila ubaguzi wa dini, kabila au asili.

Naye Mlezi wa JAI, Sheikh Alhaji Masoud, alitoa wito kwa jamii kuendelea kuishi kwa upendo, mshikamano na huruma kwa kuwajali watu wenye mahitaji mbalimbali, akisisitiza kuwa kusaidiana ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.
Awali, akisoma risala ya jumuiya hiyo, Katibu wa JAI wilayani Kasulu, Bi. Aisha Rubeni, amesema kuwa hadi sasa jumuiya hiyo imefanikiwa kutoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa 3,164. Alitoa wito kwa Serikali na jamii kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono JAI ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa makundi yenye uhitaji katika jamii.