Joy FM

Mwenge kutembelea miradi 7 ya zaidi ya bilioni 37

10 September 2026, 11:12

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, Mwl. Vumilia Julius Simbeye, amepokea Mwenge wa Uhuru, Picha na Hagai Ruyagila

Mwenge wa uhuru 2026 umeendelea na mbio zake katika Halmashauri ya mji wa Kasulu ambapo unatembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo

Na Hagai Ruyagila

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, Mwl. Vumilia Julius Simbeye, amepokea Mwenge wa Uhuru 2026 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Murufiti, Halmashauri ya Mji Kasulu.

Mkurugenzi Mwl. Vumilia Julius Simbeye amesema Mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilomita 72 na kutembelea jumla ya miradi saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 37.

Amesema baadhi ya miradi hiyo saba inahusisha sekta za afya, elimu, maji, barabara, kutawala bora na vijanaambapo baadhi itazinduliwa, mingine kutembelewa na kukaguliwa, pamoja na kuwekwa mawe ya msingi.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru umekuwa chachu ya kuhamasisha na kuibua maendeleo katika maeneo mbalimbali unapopita.

Mwenge huo unatarajiwa kutembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Halmashauri ya Mji Kasulu.