Joy FM

DC Uvinza ahimiza usafi wa mazingira

27 April 2026, 16:24

Mkuu wa Wilaya Uvinza Mkoani Kigoma Dinah Mathaman akizungumza mara baada ya zoezi la usafi wa mazingira, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Mkuu wa Wilaya Uvinza mkoani Kigoma amesema wananchi hawana budi kuzingatia suala la usafi wa mazingira ili kuhakikisha wanaepukana na mazingira ambayo yanaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Na Mwandishi wetu

Wananchi wa Wilaya ya Uvinza wameungana kushiriki shughuli za usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya ya Uvinza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Muungano, kwa lengo la kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya na kuhamasisha uwajibikaji wa pamoja kwa jamii.

Maadhimisho hayo yameongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, ambaye aliwapongeza wananchi kwa moyo wao wa kujitolea na uzalendo katika kushiriki shughuli hizo muhimu za kijamii.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mh. Dinah amewahimiza wananchi kuendelea kulinda na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni nguzo muhimu inayoiweka nchi katika hali ya utulivu, ushirikiano na maendeleo endelevu.

Mkuu wa Wilaya Uvinza akifawa na wananchi na watumishi katika zoezi la usafi wa mazingira, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Katika kuadhimisha siku hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya pia alitembelea wodi ya wazazi katika hospitali hiyo, ambapo alipata fursa ya kuwajulia hali akina mama waliojifungua na kuwapa zawadi mbalimbali. Aidha, aliwapongeza kwa ujasiri wao na kuwahimiza kuendelea kuzingatia huduma za afya kwa ajili ya ustawi wao na watoto wao.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanalala kwenye vyandarua vyenye dawa ili kujikinga na ugonjwa wa malaria, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya ya watoto na kupunguza vifo vinavyotokana na malaria.

Baadhi ya watumishi na wananchi Wilayani Uvinza wakatika zoezi la usafi wa mazingira, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza