Joy FM
Joy FM
24 June 2026, 11:52

Watumishi wa umma ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote, kwani wao ndio wanaosimamia utoaji wa huduma kwa wananchi na ni muhimu kwa mamlaka husika kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakabili zinatatuliwa kwa wakati ili kuongeza ufanisi kazini
Sadick Kibwana
Watumishi wa Umma katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati, hatua inayolenga kuboresha ustawi wao na kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.
Wito huo umetolewa katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, ambapo Halmashauri ya Mji wa Kasulu iliendesha kliniki maalumu ya siku saba kuanzia Juni 16 hadi 23 mwaka huu. Katika kipindi hicho, huduma za kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi zilitolewa katika kata saba kati ya kata 15 za halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa kufunga kliniki hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Vumilia Simbeye, amesema kuwa utaratibu wa kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi haupaswi kuishia katika wiki ya utumishi wa umma pekee, bali unapaswa kuwa endelevu ili kuimarisha mshikamano na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
Aidha, Simbeye amewakumbusha watumishi wote kuzingatia miongozo, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili waendelee kupata stahiki zao kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wao, baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu wamepongeza uanzishwaji wa huduma hiyo, wakieleza kuwa itasaidia kuimarisha mahusiano kazini, kuongeza mshikamano na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”