Joy FM
Joy FM
25 June 2026, 14:00

Ugonjwa wa kifua kikuu bado ni moja ya changamoto za kiafya zinazokabili jamii nyingi nchini Tanzania pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wa afya katika kutoa elimu na huduma za matibabu, bado baadhi ya wananchi wanaendelea kushikilia imani potofu kwamba ugonjwa huo unasababishwa na uchawi au kulogwa
Na Emmanuel Kamangu
Imani Potofu yatajwa Kuchangia vifo vya wagonjwa wa kifua kikuu KasuluImani potofu imeendelea kutajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia vifo vya baadhi ya wagonjwa wa kifua kikuu katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, mkoani Kigoma, kutokana na wananchi wengine kuamini kuwa wameathiriwa na uchawi badala ya kutafuta matibabu hospitalini.
Licha ya juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu, bado baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kufika mapema kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa sababu ya dhana kwamba ugonjwa huo unasababishwa na kulogwa.
Mratibu wa Huduma za kifua Kikuu katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Dkt. Masanja Byuram, amesema wananchi wanapaswa kuachana na imani hizo potofu kwani kifua kikuu ni ugonjwa wa kawaida unaotibika endapo utagundulika na kuanza kutibiwa mapema.
Amesema mtu yeyote anayekohoa kwa muda wa wiki mbili au zaidi anapaswa kufika katika kituo cha afya au hospitali kwa ajili ya uchunguzi na vipimo, badala ya kutumia dawa bila ushauri wa wataalamu au kuamini kuwa amelongwa.
“Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa kifua kikuu si ugonjwa wa kulogwa Serikali imeweka huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika vituo mbalimbali vya afya ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma mapema,” amesema Dkt. Byuram.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za uchunguzi wa kifua kikuu kwa kutoa vipimo bure kwa watu wote wanaoonesha dalili za ugonjwa huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuutokomeza katika jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kasulu wamesema bado kuna uelewa mdogo kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu, hali inayowafanya baadhi ya watu kutumia dawa kiholela au kuchelewa kutafuta matibabu sahihi wanapopata dalili za ugonjwa huo.Kifua kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria na husambaa kwa njia ya hewa.
Mtu mwenye maambukizi anaweza kuwaambukiza wengine anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza bila kuchukua tahadhari stahiki, hivyo elimu kwa jamii inaendelea kuwa muhimu katika kudhibiti maambukizi yake.