Joy FM

Waziri Mkuu asisitiza tafiti kuimarisha masoko

16 April 2026, 6:02 pm

Waziri Mkuu akiwa katika kongamano la biashara na uwekezaji la ziwa Tanganyika, Picha na Lucas Hoha

Waziri Mkuu wa Tanzania DKT Mwigulu Nchemba amewataka wawekezaji wa nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika kuwekeza mkoani Kigoma kwani serikali imeufungua Mkoa huo kibiashara kwa kutekeleza miradi muhimu ikiwemo kuweka umeme wa uhakika, uboreshaji wa bandari na ujenzi wa reli ya kisasa.

Na Mwandishi wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ameisisituza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, (TANTRADE) kufanya tafiti za uhakika na uchambuzi wa masoko ya bidhaa kisha kutoa taarifa kwa wafanyabiashara ili kuongeza wigo wa masoko na kufanya biashara zao kwa tija.

Waziri Mkuu ametoa ushauri huo akihutubia kongamano la Uwekezaji na Biashara kwa ukanda wa Ziwa Tanganyika, lililojumuisha wadau wa biashara kutoka ndani ya mkoa na mataifa jirani yanayopakana au kuwa na mahusiano  ya kibiashara na mkoa wa Kigoma, huku akisisitiza  kufunguliwa kwa ukurasa mpya wa kibiashara kupitia kongamano hilo.

Waziri Mkuu akizungumza mbele ya wadau mbalimbali wa uwekezaji, Picha na Lucas Hoha

Amesema serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji katika mkoa wa Kigoma ili kujenga mazingira rafiki kibiashara na kuimarisha utendaji wa sekta binafsi.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Taasisi za kifedha nchini, kukuza uwekezaji na kuendeleza biashara katika mkoa wa Kigoma ambao ni ukanda wa kimkakati katika eneo la Ziwa Tanganyika na maeneo jirani.

Waziri Mkuu akiwa katika kongamano la biashara na uwekezaji la ziwa Tanganyika, Picha na Lucas Hoha

Amewakumbusha washiriki kuwa, kongamano hilo ni mkakati wa Makusudi wa Serikali ili kuuwezesha mkoa kuwa kitovu cha biashara na kupiga hatua zaidi kiuchumi kwa manufaa ya wakazi na taifa kwa ujumla.

“Kupitia kongamano hili, tuweke utaratibu wa kukuza wigo wa ushirikiano na wadau wa kimataifa ikiwemo taasisi za kibiashara za kimataifa, wadau wa maendeleo na taasisi za fedha” amesisitiza Dkt. Mwigulu Nchemba.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Dkt. Lameck Nchemba akizungumza katika kongamano la uwekezaji na biashara Kigoma, Picha na Lucas Hoha