Joy FM
Joy FM
9 July 2026, 13:33

Kupokelewa kwa majengo ya Chuo cha Ufundi Maloregwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kunatajwa kuwa hatua muhimu itakayochochea maendeleo ya elimu na uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo
Na Mwandishi wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma, imekabidhiwa rasmi majengo ya Chuo cha Ufundi Maloregwa yaliyokuwa yakitumiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) katika iliyokuwa Kambi ya Wakimbizi ya Nduta.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika eneo la aliyekuwa Kambi ya Wakimbizi ya Nduta, wilayani Kibondo.

Akikabidhi nyaraka za majengo hayo, Afisa Msimamizi wa UNHCR, Bw. Moulid Dugsiye, amesema majengo hayo yalikuwa yakitumika kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa wakimbizi pamoja na wananchi wa jamii zinazozunguka kambi hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Mstaafu Aggrey Magwaza, amesema Serikali itaendelea kuyatumia majengo hayo ili kuendeleza dhamira ya kuanzishwa kwake, kwa kutoa mafunzo ya ufundi stadi yatakayowanufaisha wananchi.

Majengo yaliyokabidhiwa yanajumuisha madarasa, karakana za mafunzo ya vitendo pamoja na miundombinu mingine ya kujifunzia. Hatua hiyo imekuja kufuatia kufungwa rasmi kwa Kambi ya Wakimbizi ya Nduta iliyokuwa wilayani Kibondo.
Kwa ujumla, kupokelewa kwa majengo ya Chuo cha Ufundi Maloregwa ni fursa muhimu kwa Serikali ya kuendelea kuimarisha elimu ya ufundi stadi, kukuza maendeleo ya wananchi na kuhakikisha miundombinu iliyojengwa kwa ushirikiano na UNHCR inaendelea kuwanufaisha Watanzania kwa miaka ijayo.
