Joy FM

TAKUKURU yawafunda wasimamizi wa miradi Kigoma

1 July 2026, 16:59

Baadhi ya wasimamizi wa miradi Kigoma wakiwa kwenyenpicha ya pamoja na Katibu tawala Mkoa wa Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Usimamizi wa miradi ya maendeleo ni muhimu kwa ajili ya manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla

Na Mwandishi wetu

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, imeendesha warsha maalum iliyowakutanisha wadau wa usimamizi wa utekelezaji Miradi ya Maendeleo Mkoa wa Kigoma 

Warsha hiyo imelenga kuwajengea uelewa na kuweka maazimio tendaji ya pamoja kwa wadau hao, yanayolenga kufanikisha jukumu la taasisi hiyo katika kufuatilia thamani ya matumizi ya fedha na ubora katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

Akifungua Warsha hiyo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Katibu Tawala Mkoa CPSP. Hassan Rugwa amesema lengo la TAKUKURU ni kuhakikisha rasilimali za Umma zinatumika kwa malengo kusudiwa ili kunufaisha wananchi na kuleta tija kwa Maendeleo ya taifa.

Amesema mara baada ya taasisi za Umma kupokea fedha za miradi ya Maendeleo kwa kipindi cha 2026/2027, wataalam wanapaswa kufanya mapitio na kubaini hali ya kutotosheleza au utoshelevu wa fedha zilizopokelewa ili miradi iliyolengwa iweze kutekelezwa kama ilivyopangwa.

Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma Asha Kwariko, amesema kuanzia Mwaka 2023 hadi 2026, jumla ya Shilingi 321,968,816,454.76 zimeokolewa kupitia ukaguzi uliofanywa na taasisi hiyo uliohusisha jumla ya miradi 333.

Amesema katika kipindi hicho, jumla ya miradi 19 ilibainika kuwa na dosari na kuwekwa chini ya uchunguzi huku mingine 314 ilitakiwa ifanyiwe marekebisho kutokana na kuwa na mapungufu, kwa mujibu wa taratibu za kiuchunguzi za TAKUKURU.

Ameeleza kuwa, kwa Mwaka 2025/2026, Taasisi imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi Mil. 250 kutokana na kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya dosari zilizobainika katika baadhi ya miradi mkoani Kigoma.

Upande wake Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma Vedastus Mazuge, amesema iwapo Halmashauri zitafanya ufuatiliaji na Tathmini pamoja na uwepo wa uwajibikaji kwa viongozi na watendaji, changamoto hizo zitapungua kwa kiasi kikubwa na hata kumalizika kabisa.

Amezitaja baadhi ya changamoto zilizobainishwa na taasisi hiyo kuchangia dosari kwenye utekelezaji miradi ya Maendeleo ni pamoja na kutoshirikishwa kwa wananchi wakati wa uibuaji miradi, uchepushaji wa fedha, uwepo wa miradi hewa, manunuzi na matumizi ya fedha yasiyozingatia taratibu.